Kuhusu
Historia ya Seminari
Jinsi Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria Visiga ilivyoanzishwa, na magombera walioiongoza tangu 1990.
Wazo la kuanzisha seminari
Nia na lengo la kuanzisha seminari
Tarehe 25/05/1969 sikukuu ya Pentekoste, Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa alitawazwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, akimpokea ambaye sasa ni marehemu, Askofu Mkuu Edgar Maranta, wa shirika la Makapuchini kutoka Uswisi. Alipofika Jimboni D’Salaam kuanza kazi yake ya kiaskofu alikuta mapadre wanne tu wa kiafrika wa Jimbo ambao ni Pd. Gregory Mpanda - Parokiani Kipatimu, Pd. Hermenegild Muba - huko Mahenge, Pd. Nicas Kipengele - Seminari ndogo ya Mt. Petro na Pd. Desderi - Parokia ya Mt. Petro Dar es Salaam.
Suala hili la kuwepo Mapadre wachache katika Jimbo la Dar es Salaam lilikuwa wazo la Mwadhama la kuwa na Seminari katika Jimbo lake la Dar es Salaam.
Wazo hilo lilijirudia tena wakati ambapo Baraza la Maaskofu Tanzania (T.E.C ) lilipoamua pia kujenga Seminari kuu jijini kati ya miaka ya 1970-1976 ambalo lilikabidhiwa Jimbo kuu kutafuta mahali pa kujenga hiyo Seminari. Lakini wazo lake hilo halikuweza kutengemaa licha ya kuwa alisaidia kutafuta eneo la Seminari kuu.
Mwadhama hakukata tamaa, bali aliendelea kuijengea hoja nzito nia yake hiyo kwa kutafuta sababu za kumsukuma kuwa na Seminari yake. Nazo ni zifuatazo:
- Kuzaliwa kwa Jimbo jipya la Mahenge ambalo lilikuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambamo Seminari ya Jimbo (la Dar es Salaam na Mahenge) ilikuwa imejengwa. Kwa hiyo baada ya Mahenge kuwa Jimbo, ile Seminari ndogo iliyokuwa imejengwa kule ikawa ya Jimbo la Mahenge na siyo ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Jimbo la Dar es Salaam likawa halina Seminari tena.
- Pia matatizo katika Seminari ndogo ya kanda iliyopo Morogoro yalichangia kwa kiasi kikubwa Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa kusisitiza na kuona kwamba wazo lake lilikuwa na umuhimu mkubwa sana.
- Ufunguzi wa Seminari ndogo katika majimbo mengine, ulichangia kwa kiasi kikubwa sana kuimarika kwa wazo la Kardinali.
- Jimboni Dar es Salaam miito ilionekana kuwa mingi na hivyo ilionekana kuwa jambo la kusikitisha iwapo miito yote hii ingeachwa ipotee bila kulelewa.
- Upatikanaji wa eneo lililofaa kwa ukuzaji wa miito ulichangia sana kukuza wazo la Mwadhama kwani pale mwanzo eneo lilikuwa linaleta utatanishi.
- Pia suala la uongozi lilichukuliwa kama kikwazo cha kuanzisha Seminari kwa sababu walifikiri kuwa ingekuwa vigumu sana kupata uongozi mzuri wa Seminari. Lakini Mwadhama aliwaambia kuwa ameshaomba shirika Jeswiti wakamwambia kuwa watampatia mapadri ambao watasaidia kiuongozi.
Ufunguzi wa seminari
Seminari ndogo ya Mtakatifu Maria, Visiga ilifunguliwa rasmi mnamo tarehe 9 Mei, 1990. Mgeni rasmi katika ufunguzi huo alikuwa Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa ambaye ndiye aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa wakati huo.
Ufunguzi huo ulihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo mapadri kutoka katika parokia mbalimbali za Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Waseminari wa mwanzo
Kundi la kwanza - mwaka 1990
Suala la upatikanaji wa wanafunzi katika seminari hii ya Mtakatifu Maria ilikuwa ni kwa kutumia utaratibu wa kawaida, kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Miito na baadaye kupitia maparoko ambao walipewa jukumu la kuwatafuta vijana katika parokia zao ambao walikuwa na moyo na sifa za kujiunga na Seminari na kuwapatia fomu. Wengi kati ya hawa walipewa mtihani wa mahojiano. Hatimaye wale waliofaulu mtihani wa mahojiano walipewa mtihani wa kuandika.
Kundi kubwa la wanafunzi walipatikana kutokana na mtihani ule walipelekwa katika Seminari ya Mtakatifu Petro iliyoko huko Morogoro na waliobaki waliletwa katika Seminari ya Mtakatifu Maria 20 April, 1990. Wanafunzi hao wa kwanza idadi yao ilikuwa ni wanafunzi kumi na nane.
Gombera aliyewapokea wanafunzi hawa alikuwa Padri Henry Mrema.
Vijana hao waliopatikana hawakuanza masomo yao ya kidato cha kwanza rasmi bali walianza na “Pre-Form One” ambapo walijishughulisha na sala, kazi za mikono na baadhi tu ya masomo.
Sababu zilizowafanya wasianze moja kwa moja na masomo yao ya kidato cha kwanza zilikuwa kama zifuatavyo:
- Kutokamilika kwa uongozi wa shule; kwa mfano, kulikuwa na upungufu wa mapadri, walimu na wahudumu mbalimbali, hii ndio iliyokuwa sababu kubwa ya kimsingi.
- Ukosefu wa vitabu vya kiada na ziada.
- Ukosefu wa maktaba kamilifu yenye vitabu vyote vyakuweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi kimasomo.
II. Kundi la pili mwaka 1991
Mnamo mwaka 1991 walipatikana wengine wachache waliojiunga na wenzao walioanza tangu mwaka 1990 na kuunda darasa moja, lenye wanafunzi thelathini na watano (35).
Darasa la kwanza la Seminari ya Mtakatifu Maria lilianzishwa mwaka 1991 likiwa na jumla ya wanafunzi thelathini na watano (35). Kati ya hawa, wanafunzi kumi na nane (18) walitokana na dirisha la usaili lililofanyika katika Seminari ya Mtakatifu Petro mwaka 1990. Wanafunzi hao waliletwa kuendelea na masomo yao katika Seminari ya Mtakatifu Maria tarehe 20 Aprili, 1990.
Mnamo mwaka 1991, wanafunzi wengine kumi na saba (17) walijiunga rasmi na seminari hii, na hivyo kuunda darasa kamili la kwanza lenye wanafunzi thelathini na tano (35) walioungana kwa pamoja mwaka huo wa masomo.
Wanafunzi hao walipokelewa na Gombera wa kwanza, Mheshimiwa Padre Henry Mrema.
Mwaka 1991, Padre Melchior Gutambi alishika nafasi ya ugombera ambayo hapo awali ilikuwa imeshikwa na Padri Henry Mrema. Chini ya uongozi wa Padri Gutambi, Seminari ilianza kupata walimu waliosaidia kufundisha kwa muda. Walimu hawa walikuwa ni vijana (walimu) kwa mujibu wa sheria kutoka Ruvu J.K.T. na wengine kutoka Ruvu Sekondari.
Zaidi ya hao, walipatikana walimu wa kudumu kama vile mwalimu Michael Msaki pamoja na mwalimu Leornard Mahinya ambao wote walifika mwaka 1991.
Masomo yalianza rasmi kama kidato cha kwanza mwaka 1991 chini ya uongozi wa Padri Melchior Gutambi, wakiwepo wanafunzi 35 wa Kidato cha kwanza, walimu wa muda na wachache wa kudumu. Walimu wa kudumu walikuwa ni pamoja na Padri Melchior Gutambi, Padri Venance Tegete, Padri Philipo Mkude, mwalimu Michael Msaki na mwalimu Leornard Mahinya.
C. Uongozi wa seminari
Kwa kawaida, uongozi katika seminari umegawanyika katika ngazi mbalimbali kulingana na majukumu na nafasi za viongozi.
Ngazi ya juu kabisa ni ya Gombera, ambaye ndiye padre mkuu anayesimamia seminari nzima.
Ngazi ya pili ni ya Gombera Msaidizi, ambaye pia ni padre. Mbali na nafasi hizi kuu mbili, kuna mapadre wengine wanaoshughulikia masuala mbalimbali ndani ya seminari, kama vile Padre wa Kiroho anayehusika na ustawi wa kiroho wa waseminari. Pia, kunaweza kuwa na mapadre wengine pamoja na walimu.
1. Seminari ya Visiga chini ya Gombera wa kwanza, Padre Henry Mrema, 1990 - 1991
Gombera wa kwanza kuongoza Seminari ya Visiga alikuwa Padre Henry Mrema kutoka Shirika la Opus Spiritus Sanctus (O.S.S). Alifika katika Seminari ya Visiga na kuchukua nafasi ya Gombera mwaka 1990, kabla ya wanafunzi wa kwanza kufika.
Wakati wa uongozi wa Padre Mrema kama Gombera, uongozi haukuwa umejitosheleza kwani hakukuwa na Gombera Msaidizi wala Padre wa Kiroho kwa ajili ya waseminari. Pia, walimu walikuwa wachache sana na hawakutosheleza mahitaji ya ufundishaji.
Aidha, Padre Mrema alikuta kuwa Seminari ya Visiga haijakamilika katika maeneo kadhaa: kanisa, jengo la utawala, maktaba, bwalo la chakula kwa wanafunzi, nyumba za walimu, na hakukuwa na miradi kama bustani au mifugo kama ng’ombe na nguruwe. Licha ya kukaa muda mfupi katika seminari, alijitahidi kuendeleza ujenzi wa maeneo mbalimbali katika Seminari ya Visiga.
Alijitahidi kukamilisha miundombinu kama mabweni ya kulala, nyumba za wapishi, choo cha wanafunzi (shimo), na kujenga nyumba ya mwalimu ambayo kuanzia 1991 hadi 1997 ilitumika na mwalimu Patrick Sangu. Pia, alipanda miti ya matunda kama machungwa.
Katika kipindi chote cha uongozi wake, Padre Mrema alishirikiana na Padre Mkude aliyekuwa akimsaidia katika shughuli mbalimbali.
Baada ya kuondoka, Padre Mrema alimkabidhi uongozi Padre Venance Tegete kama Gombera wa muda.
II. Uongozi wa seminari chini ya Gombera wa pili, Padre Melchior Gutambi, 1991 - 1994
Mara baada ya kuondoka kwa Gombera wa kwanza, Padre Mrema, Padre Venance Tegete alikaimu nafasi ya Gombera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria, Visiga.
Katika kipindi hiki kifupi cha kukaimu, Padre Venance Tegete alitekeleza shughuli mbalimbali katika seminari. Baadhi ya shughuli hizo ni kupanda michikichi na michungwa, pamoja na kusafisha na kuandaa mazingira yote ya seminari.
Mnamo tarehe 14 Julai, 1991, Padre Melchior Gutambi, Gombera wa pili wa Seminari ya Visiga, alipata uteuzi rasmi wa kuwa Gombera. Alifika rasmi katika Seminari ya Visiga mwezi Septemba 1990. Alikuta Seminari ya Visiga ikiwa bado haijakamilika katika maeneo mbalimbali.
Alisaidia katika usajili wa seminari ambao haukuwa umefanyika. Kama ilivyo kawaida kwa seminari zote nchini, Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria, Visiga ilisajiliwa kitaifa chini ya mtaala wa kidini, si wa kilimo wala sayansi.
Alikamilisha ukumbi wa shule ambao haukuwa umemalizika kwa kuweka paa na milango. Kanisa lililoanzishwa kujengwa chini ya uongozi wa Padre Mrema lilikamilika na kuanza kutumika na jumuiya yote ya Visiga. Kabla ya hapo, ibada na sala zote zilikuwa zikifanyika katika darasa moja la kidato cha kwanza.
Alianzisha ujenzi wa zahanati kwa sababu zahanati ya awali ilikuwa ndani ya bweni la wanafunzi, chumba namba 31. Alikamilisha ujenzi wa zahanati iliyopo nje ya mabweni ya wanafunzi, hivyo kurahisisha utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa kijiji. Vilevile, alijitahidi kumalizia nyumba mbili za walimu na kufanya jumla kuwa nyumba tatu.
Jengo la utawala lilikamilika na kuanza kutumika kama ofisi ya Gombera, ofisi ya mhasibu, ofisi ya walimu, na maktaba ya shule.
Hapo awali, waseminari hawakuwa na jikoni wala bwalo la chakula kwa kuwa havikuwa vimekamilika. Kwa hiyo, Padre Gutambi alikamilisha jikoni pamoja na bwalo la wanafunzi. Pia, hakukuwa na miradi ya mifugo katika seminari. Kwa kushirikiana na uongozi wake na Jimbo, Padre Gutambi alianzisha ujenzi wa banda la mifugo kwa ajili ya wanyama kama ng’ombe, mbuzi na nguruwe. Aliweka pia nguzo za taa kuzunguka baadhi ya majengo ya seminari kwa ajili ya usalama.
Pamoja na jitihada hizo, aliingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya C.M.C. kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira na kupiga lami barabara inayoingia katika seminari kutoka barabara kuu ya Morogoro. Hata hivyo, mkataba wa kupiga lami haukukamilika kwa sababu zisizokuwa ndani ya uwezo wake. Kampuni hiyo ilikamilisha uwanja wa mpira ambao bado unatumika hadi leo.
Katika masuala ya kitaaluma, alisaidia kupata walimu wa kawaida waliokuwa wakisaidia waseminari: Frt. Mathias Mambo na Frt. Benedict Shayo.
Katika kipindi chake cha miaka mitatu kama Gombera, mojawapo ya majanga makubwa yaliyotokea ni ajali ya gari ambapo wanafunzi saba na mlinzi mmoja walifariki dunia. Wanafunzi hao walikuwa wakipelekwa Hospitali ya Tumbi usiku kwa ajili ya matibabu ya malaria kali.
Gari la seminari lilipata ajali mbaya eneo la Miembe Saba, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, mnamo tarehe 4 Septemba 1991, siku ya maombolezo. Mazishi ya wanafunzi saba yalifanyika katika makaburi ya Msimbazi yaliyopo Parokia ya Msimbazi (Kanisa la Mama Yetu wa Fatima) jijini Dar es Salaam, isipokuwa Gabriel Mahulu na Abraham Chacha.
Baada ya ajali hii mbaya, Padri Gutambi alipumzika kwa muda na hivyo kukaa Jimboni kwa muda wa miezi michache kabla ya kurudi tena katika uongozi wake.
Baada tu ya kuondoka kwa Padri Gutambi, Padri Venance Tegete ambaye alikuwepo bado Seminarini alishika tena kwa muda nafasi hiyo ya Ugombera mara ya pili kwa miezi michache kabla ya kurudi tena kwa Padri Gutambi.
III. Seminari chini ya Gombera wa tatu. Padri Stephen Mosha (A.J) 1994 - 1996
Naye Padri Gutambi aliendelea tena na uongozi huo hadi mwaka 1994 ambapo alihamishiwa katika Seminari ya Mtakatifu Petro Morogoro, na hivyo Padri Stephen Mosha wa Shirika la Mitume wa Yesu (A.J) aliteuliwa kuwa Gombera wa tatu.
Gombera wa tatu wa Seminari ya Visiga alikuwa Padri Stephen Mosha (A.J) kutoka Shirika la Mitume wa Yesu (Apostles of Jesus). Padri Mosha alifika Seminarini Visiga mwezi Aprili mwaka 1994 na alikabidhiwa rasmi madaraka kama Gombera wa Seminari ya Mama Maria mwezi Julai mwaka 1994 na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Polycarp Pengo.
Katika kipindi hiki cha kuja kwake Seminarini Visiga, kulikuwa na idadi ya Mapadri wawili. Masista wanne, walimu 3 na wanafunzi 117. Wakati Padri Stephen Mosha alipofika alikuta Seminari ikiwa na miradi ya mifugo kama vile ng’ombe, nguruwe, mbuzi, kuku, kondoo, bata na kanga na miti ya matunda kama vile michungwa, minazi, miembe na mikorosho.
Vile vile Seminari ilikuwa na kanisa lililokamilika, bwalo, mabweni nane yenye vyumba thelathini na mbili, madarasa manne (kidato cha kwanza hadi nne) na maabara tatu, lakini kwa wakati ule ilikuwa ikitumika moja tu kati ya hizo; jengo la utawala, ukumbi ambao ulikuwa bado haujaanza kutumika, nyumba tatu kwa ajili ya walimu pamoja na jengo la zahanati ambalo lilikuwa bado halijakamilika. Katika kipindi hiki alichowasili wanafunzi pamoja na wanakijiji walikuwa wakitibiwa kwenye moja ya bweni hili lilitumika kama Zahanati.
Kwa upande wa usafiri, Seminari hii ilikuwa na lori moja na dogo ambalo lilikuwa limepata ajali na hivyo kutokutumika kwa kutoa huduma.
Katika kukaa kwake Seminarini kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kama Gombera, alifanikiwa katika nyanja mbalimbali kama vile miradi.
Kwa upande wa mifugo, Padri Stephen Mosha alifanikiwa kuongeza idadi ya mabanda ya mifugo na kufikia mabanda matano. Pia aliongeza idadi ya mifugo na alinunua mashine ya kukatia majani ya ng’ombe pamoja na jembe la kukokotwa na ng’ombe.
Kwa upande wa kilimo alifanikisha uongezaji wa bustani za mboga na matunda, upanuzi wa mashamba na kilimo cha mazao kama mahindi na mihogo.
Katika kipindi cha uongozi wake, Padri Stephen alifanikisha ujenzi wa vitu mbalimbali ambavyo havikuwepo kabla ya uongozi wake. Alifanikisha ujenzi wa stoo kubwa ya kuhifadhia vitu mbalimbali vya shule hasa vyakula.
Idadi ya nyumba za walimu iliongezeka kwa ujenzi wa nyumba mbili zaidi.
Pia alifanikisha ujenzi wa mtambo wa gesi (Biolatrine Gas) ambao unatoa nishati ya gesi katika majiko ya mapadri na wanafunzi.
Mbali ya ujenzi na upanuzi wa vitu mbalimbali, Padri Stephen alifanikisha ufunguzi rasmi wa vitu mbalimbali kama Zahanati ya shule ambayo ipo nje ya mabweni ya wanafunzi, ukumbi wa shule ambao ulikuwa umekamilika lakini bado kuanza kutumika na nyumba ndogo ya ukarabati wa samani mbalimbali hapa Seminarini.
Kwa upande wa usafiri ambao hapo awali ulikuwa tatizo kubwa, Padri Stephen alifanikisha upatikanaji wa magari ya shule, akisaidiwa na Jimbo, ambalo lilitoa fedha za kununulia “Toyota Land Cruizer” TZG 5293 na kupatiwa msaada na Makapuchini wa Dar es Salaam ambao walisaidia upatikanaji wa lori dogo tani 3½ aina ya Mitsubishi TZJ 6492.
Kabla ya uongozi wake, hakukuwa na mpango wa kuwa na sare moja kwa wanafunzi wote, lakini kwa kipindi chake alijitahidi katika suala hili la sare ambapo wanafunzi walianza na mashati meupe ya mikono mirefu na suruali nyeusi. Hapo awali hapakuwa na Baraza la wazazi na siku ya wazazi (Parents) hapa Seminarini, kwa jitihada za uongozi wake alifanikisha uanzishaji wa Baraza hilo na siku hiyo ya wazazi.
Baraza hili la wazazi limefanikiwa kujenga uhusiano wa karibu kati ya uongozi wa Seminari, waseminari kwa ujumla na wazazi wenyewe.
Uhusiano huu umefanikisha upatikanaji wa vitabu mbalimbali vya masomo, vifaa mbalimbali vya maabara na uongezaji wa walimu hapa Seminarini; hadi kufikia walimu (10).
Kutokana na jitihada zake nyingi kitaaluma, alifanikiwa kuiwezesha shule kuwa na matokeo mazuri ya kidato cha nne kwa mwaka wa kwanza wa kipindi cha uongozi wake (1994) shule ilishika nafasi ya sitini na moja (61) kitaifa, mwaka wa pili (1995) shule ilishika nafasi ya ishirini na mbili na kwa mwaka wa mwisho wa uongozi wake (1996) shule ilishika nafasi ya tano kitaifa na mwaka 1997 shule ilikuwa ya tano kutokana na msingi mzuri aliouweka.
Zaidi ya mafanikio yake makubwa hayo, katika kipindi chote cha uongozi wake, Padri Stephen Mosha alikumbana na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa mawasiliano ya haraka na mjini hususni simu. Licha ya kufanikisha ujenzi wa nyumba mbili za walimu, bado kulikuwa na upungufu wa nyumba za walimu.
Padri Stephen alikaa Seminarini Visiga kwa muda wa miaka miwili na nusu. Baada ya kuondoka kwake, nafasi yake ilishikwa na Padri Venace Karobo Twinomuhenzi (A.J) ambaye alifika mnamo mwezi Novemba mwaka 1996 kama Gombera wa nne.
IV. Uongozi wa seminari chini ya Gombera wa nne, padri Venance Karobo Twinomuhenzi – Novemba 1996 – Novemba 1997
Padre Venance Karobo aliwasili Visiga tarehe 23 Novemba, 1996. Alitoka katika Shirika la Mitume wa Yesu (Apostles of Jesus).
Alikuta jumla ya wanafunzi 96. Kidato cha kwanza walikuwa 31, Kidato cha cha pili 32 na Kidato cha tatu 33. Kidato cha Nne walikuwa wamekwisha ondoka. Pia alikuta walimu 13 ambao kati yao 10 walikuwa walimu walei na mapadre watatu. Hakukuta frateri yeyote hapa Seminarini.
Walimu aliowakuta ni Mwalimu Patrick Sangu, Mwalimu Beatus Nguge, Mwalimu Mushumbusi Gosbert. E, Mwalimu Sylvester Mbao, Mwalimu Michael Msaki, Mwalimu Blasdius Matangalu, Mwalimu John Brash, Mwalimu Whilhem Ringia, Mwalimu Gisbert Mtumbuka na Mwalimu Alfred Rwegoshora.
Mapadre ambao aliwakuta ni Pd. Mathias Mambo, Pd. Martin Dominic na Pd. Richard Ntambazi.
Kuna mafanikio mengi ambayo yalipatikana wakati wa kipindi chake cha uongozi. Chumba cha jiko cha mapadre kiliongezwa, mabweni ya wanafunzi yalikarabatiwa na nyavu mpya za madirisha kuwekwa. Hii ilipunguza sana ugonjwa wa Maralia hapa Seminarini.
Josho kwa ajili ya wanyama lilijengwa. Wakati wa kipindi cha uongozi wa Pd. Venace Karobo. Matokeo ya mtihani yalikuwa ni yakuridhisha. Katika mtihani huo wa Taifa wa kidato cha Nne shule ilikuwa ya tano. Vile vile wodi ya wanafunzi wagonjwa ilianzishwa.
Wakati wa uongozi wa Pd. Venace Karobo kuna matatizo machache yalitokea. Mojawapo ya matatizo makubwa yaliyokuwepo ni uongozi mbaya wa wanafunzi. Hii ilisababisha uongozi huo kuondolewa na uongozi mpya wa wanafunzi kuchaguliwa na kamati ya walimu na mapadre.
Tatizo lingine ni kwamba koo cha gari kilivunjwa kutokana na jaribio la wezi kutaka kukiiba. Kioo hicho kilikuwa cha Lori dogo tani tatu na nusu, aina ya Mistubishi yenye namba za usajili TZJ 6492.
Padre Venace Karobo aliongoza Seminari kwa muda wa mwaka mmoja wa masomo. Baada ya kuondoka kwake nafasi yake ilichukuliwa na Pd. Euzebius Nzingilwa.
V. Uongozi chini ya Gombera wa Tano Padre Eusebius Nzingilwa DEC 1997 - SEPT 1999
Baada ya kumalizika kwa uongozi wa awamu ya nne katika Seminari ya Visiga, Baba Askofu alifanya mabadiliko katika mfumo mzima wa uongozi wa Seminari. Kufuatia mabadiliko hayo, uongozi uliwekwa mikononi mwa Mapadre wa Jimbo. Hivyo, Mapadre wa shirika waliokuwepo waliondoka na nafasi zao kuchukuliwa na Mapadre wa Jimbo.
Mapadre wa shirika waliohamishwa kutoka Seminari ya Visiga walikuwa ni Padre Venance Karobo, ambaye alikuwa Gombera wa Seminari hii hapo awali, na Padre Richard Ntambazi, ambaye alikuwa Baba wa Roho, wote kutoka Shirika la Mitume wa Yesu (Apostles of Jesus).
Pia kutokana na mabadiliko ya uongozi, Padre Martin Dominic, ambaye alikuwa Gombera Msaidizi, alihamishwa kutoka Seminari ya Visiga na kuwa mlezi katika nyumba ya malezi iliyoko Kunduchi–Mtongani na kupewa wadhifa wa Mkurugenzi wa Miito katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Katika zoezi zima la kuweka uongozi wa Seminari ya Visiga chini ya Mapadre wa Jimbo, baadhi ya Mapadre wa Jimbo walihamishiwa katika Seminari hiyo. Mapadre hao ni pamoja na Padre James Mweyunge na Padre Eusebius Nzingilwa, ambaye hapo awali alikuwa mlezi katika nyumba ya malezi iliyoko Kunduchi–Mtongani.
Padre Eusebius Nzingilwa, Gombera wa tano wa Seminari ya Visiga, aliwasili hapo Seminarini mnamo tarehe 15 Desemba, mwaka 1997. Alikuta jumla ya wanafunzi themanini (80), walimu walei kumi (10), Frater mmoja (1), Masista watano (5) pamoja na Padri mmoja (1).
Padri mmoja aliyekuwepo alikuwa Padre Mathias Mambo, ambaye alikuwa Gombera Msaidizi na Baba wa Roho.
Padre Eusebius Nzingilwa alifika pamoja na Mapadre wengine wawili—Padre James Mweyunge anayeshughulikia masuala ya nidhamu na Padre Paul Njoka anayeshughulikia masuala ya kazi na miradi. Hivyo, idadi ya Mapadre katika Seminari ya Visiga ikafikia wanne.
VI. Uongozi chini ya Gombera wa sita Padre Mathias Mambo. Sept 1999 - July 2003
Seminari ndogo ya Mt. Maria – Visiga ilikuwa chini ya uongozi wa Pd. Euzebius Nzigilwa kama Gombera kuanzia Januari 1998 hadi Septemba 1999. Hivyo Pd. Nzigilwa aliongoza seminari kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
Pd. Nzigilwa alikuwa Gombera wa tano wa seminari hii ndogo ya Mt. Maria–Visiga. Katika uongozi wake, seminari ilipata mafanikio makubwa. Shule ilipata kisima cha kuhifadhi maji na kuchimba visima viwili vya maji vinavyosaidia katika umwagiliaji na matumizi mengine. Pia alifanikiwa kuleta Dish na Runinga kwa ajili ya seminari. Pia kulikuwa na maendeleo mengine madogo madogo hasa katika taaluma, kazi, malazi, michezo, afya na malezi kwa ujumla ambayo Pd. Nzigilwa alijitahidi kuyaboresha. Matatizo madogo ya hapa na pale hayakosekani.
Kwa sasa, Seminari ndogo ya Mt. Maria–Visiga ipo chini ya uongozi wa Pd. Mathias Mambo kama Gombera wa sita. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimteua Pd. Mambo kushika uongozi wa seminari mara baada ya Pd. Nzigilwa kwenda masomoni.
Alipochukua rasmi uongozi wake tarehe 13/08/1999 kama Gombera wa sita, Pd. Mambo aliwakuta mapadre wengine watatu, masista watano, wafanyakazi wapatao thelathini, na waseminari wanafunzi 126.
Kazi na mafanikio yake
Padre Mathias Mambo kama Gombera, alishirikiana na mapadre wengine, masista na wafanyakazi na kufanikisha kwa kiasi kikubwa kuboresha miradi, ujenzi wa majengo mbalimbali, taaluma, afya na michezo. Kwa upande wa miradi, Pd. Mambo alifanikiwa kujenga banda moja la kuku ambalo tayari limeshaanza kutumika. Pia amefanikisha kujenga na kukarabati majengo mbalimbali.
Mtazamo wa jimbo kuu kuhusiana na seminari yake
Jimbo Kuu la Dar es salaam chini ya Askofu Mkuu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo lina mitazamo mbalimbali kuhususiana na Seminari yake ndogo ya Mtakatifu Maria – Visiga.
Mojawapo ya mitazamo ya Jimbo Kuu ni kuiendeleza zaidi.
- Kitaaluma
- Kuisadia iweze kujitegemea
- Umalizaji wa ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali Seminarini ili kufanikisha lengo lake jema la kupata Mapadri bora.
Kitaaluma
Walezi:: Ni muhimu na wana jukumu kubwa katika malezi ya waseminari kama walimu. Hata hivyo ni vyema kuwa Mapadri wa kutosha seminarini. Seminari ya Mtakatifu Maria Visiga ambayo iko chini ya mojawapo ya sababu kuu zinazofanya Jimbo Kuu la Dar es salaam lilichelewa kutimiza azma yake kuanzisha kidato cha tano na cha sita ni hizi zifuatazo:
Uchache wa waseminari kwa vidato hivyo
Idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Seminari hapa nchini kwa kidato cha tano na cha sita kwa nia ya kuwa mapadre ni chache zaidi kulinganisha na idadi ya Seminari zilizopo hapa nchini kwetu
Kwa Jimbo Kuu la Dar es salaam kutokana na hali hii ilivyo hapa nchini ni vigumu kuanzisha kidato cha tano na cha sita kwa sasa hivi. Hii nii kutokana na uchache wa wanafunzi ambao hawatafikia idadi inayohitajika katika darasa.
Uchache huu wa waseminari unasababishwa na mambo mbalimbali.
- Maadili: Baadhi ya waseminari hawaendelei na masomo yao katika Seminari kutokana na kutokuwa na maadili mazuri.
- Tabia/nidhamu: Tabia/Nidhamu (sala, kazi, michezo, Ratiba/Utaratibu): Tabia nzuri na nidhamu ni wajibu wa kila Mseminari kuonyesha katika maisha yake yote na hasa awapo katika mazingira ya shule/Seminarini hali hiyo inatakiwa kuonekana katika sala, kazi, michezo na kufuata ratiba/utaratibu, hivyo kushindwa kwa waseminari kufuata utaratibu mzima wa Seminari wanazosoma hukuta wanajifukuzisha shule na kushindwa malengo yao.
- Kutokuwa na wito: Ni kweli kwamba hakuna chombo ambacho mtu anapimwa kama ana wito au hana, lakini kuna vitu anavyoweza akawa anavifanya na hivyo kugundua kwa urahisi kabisa kama mtu huyo ana wito wa kuwa Padri au hana, hivyo anapogundulika mara moja mtu huyo hushauriwa kufuata njia nyingine ya maisha.
- Kitaaluma: Kwa upande wa kitaaluma Seminari zina kiwango cha wastani wa masomo ambacho mseminari ana lazimika kukifikia kwa kila muhula. Kwa wale wachache ambao wanashindwa kufikia kiwango hicho kitaalamu wanapewa uhamisho kwenda shule nyingine na hivyo kushindwa kufanikisha malengo yao.
- Mikondo: Idadi kubwa ya Seminari hapa nchini hazina mikondo ya sayansi kama PCB, PCM, PBG Na EGM hivyo kufanya idadi ya Waseminari kuwa chache kwa sababu baadhi yao wanashindwa kujiunga na Seminari hizi za kidato cha tano na cha sita kwa kukosa mikondo ya masomo wanayopendelea.
Sababu zote hizi zinachangia kwa kiasi kikubwa sana kuwapo kwa upungufu mkubwa wa seminari walio tayari kujiunga na Seminari hizi kwa kidato cha tano na cha sita.
Hivyo basi kuanzisha kidato cha tano na cha sita italigharimu Jimbo Kuu gharama kubwa kulinganisha na idadi ya wanafunzi kwa vidato hivyo hususan malipo kwa walimu wa vidato hivyo.
Seminari zenye kidato cha tano na cha sita ni nyingi
Hapa nchini kuna Seminari nyingi za Kidato cha tano na cha sita wakati idadi ya wanafunzi wanaojiunga katika Seminari ni chache zaidi.
Mtazamo wa Jimbo wa kuanzisha kidato cha tano na cha sita katika Seminari yake ndogo ya Mtakatifu Maria utapunguza hata ile idadi ndogo ya wanafunzi wanaoenda katika Seminari hizo kwa sasa.
Wazo kuu la Maaskofu wa Tanzania ni kuimarisha Seminari hizi za kidato cha tano na cha sita zilizoko nchini ili ziweze kufikia kiwango kinachoridhisha kabisa kitaaluma. Kuziweka Seminari hizi katika mazingira mazuri ili kuwawezesha waseminari kusoma vizuri ni mtazamo unaopewa kipaumbele na Maaskofu hawa wa Tanzania.
Gharama kubwa za kuanzisha vidato hivyo
Vilevile Jimbo Kuu linatambua upungufu mkubwa wa vifaa vya maabara na vitabu vya kiada na ziada ambavyo Seminari yake ndogo inakabiliwa nao. Hivyo basi vinajitahidi sana kukabiliana na tatizo hilo kwa namna mbalimbali kabla ya kuanza mipango ya ujenzi wa kidato cha tano na cha sita.
Hata hivyo Jimbo Kuu bado lina upungufu wa fedha za kutosha za kuweza kuwalipa walimu wa ngazi ya chuo kikuu, kununua vitabu vya vidato hivyo ambavyo idadi yake kubwa ni vyakuagizwa kutoka nje vya nchini bei yake ni kubwa, vile vile gharma ya madawa, vifaa na kemikali za maabara ni kubwa mno.
Jimbo Kuu pia lina upungufu wa fedha za ujenzi wa Mabweni, Madarasa, Maabara na hata Maktaba kwa ajili ya vidato hivyo.
Kuisaidia seminari ili iweze kujitegemea
Jimbo Kuu lina mitazamo mbalimbali ya kuifanya Semiari yake ijitegemee kwa nyanja mbalimbali ili kujaribu kupunguza gharama za uendeshaji, hivyo limejaribu kuisaidia miradi ifuatayo:
- Biolatrine Gas: Katika siku za karibuni Seminari ikishirikana na Jimbo imeweza kujijengea Mtungi wake wa Gesi (Biolatrine Gas). Kwa namna moja ujenzi wa Mtungi huu umepunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya mkaa na umeme.
- Kisima cha maji: Jimbo linatazamia kuchimbia kisima cha maji ambacho kitapunguza gharama inayoikabili Seminari hii. Kufanikiwa kwa suala hili kunatazamiwa kuleta maendeleo ya shughuli mbalimbali hapa Seminarini kwa ufugaji na kilimo cha umwagiliaji mashamba na bustani pamoja na matumizi mengine ya binadamu.
- Zahanati: Kwa upande wa zahanati ambayo Seminari inayo, Jimbo Kuu likishirikiana na Seminari imejaribu kwa kiasi fulani kupunguza gharama za uendeshaji wake kwa kuwaruhusu wakazi wa kijiji cha Visiga kujipatia huduma za matibabu kwa malipo nafuu. Hivyo fedha hizo ndizo zinasaidia kuiendesha Zahanati hiyo, kwa kuwahudumia Waseminari wake, Wafanyakazi wake, Mapadre na Mastista bure.
- Kilimo: Seminari imeweza kutumia sehemu ya eneo lake kwa shughuli za kilimo. Mazao ambayo yanalimwa kwa kiasi kikubwa Seminarini ni mihogo, viazi vitamu, mipapai, kunde, michungwa na minazi.
- Ufugaji: Vilevile kwa upande wa mifugo Seminari inajitegemea katika sekta hii kwa kiasi kikubwa. Imeweza kujijengea mabanda ya mifugo mbalimbali. Mifugo ambayo inafugwa seminarini Visiga ni ng’ombe, mbuzi, ngurwe, kuku, bata, sungura na kanga.
Hivyo kujitegemea kwa seminari kutafanikiwa endapo jumuiya yote inayoishi hapo Seminarini itawajibika ipasavyo katika nyanja zote kama vile kilimo, kitaaluma na katika utatuzi wa matatizo madogo yanayoikabili jumuiya nzima kwa ujumla.
C: Ujenzi na ukarabati wa majengo
Licha ya mitazamo na mipango mbalimbali ya Jimbo Kuu kuiendeleza Seminari yake Kitaaluma na katika suala la kujitegemea pia lina mipango kuhusiana na ujenzi.
i. Ujenzi wa Majengo
Katika kipindi cha ukarabati, Jimbo Kuu likishirikiana na uongozi wa Seminari limeweza kufanya ujenzi wa vitu mbalimbali muhimu hapa Seminarini. Jimbo Kuu limeweza kujenga nyumba za walimu. Vile vile limeweza kujenga ghala kubwa kwa ajili ya kuhifadhi vitu mbalimbali na hasa chakula cha wanafunzi pamoja na ujenzi wa mabanda ya mifugo (Nguruwe na Ng’ombe).
Kwa siku za usoni Jimbo Kuu linatazamia kuongeza majengo mbalimbali ili kuufikia kiwango kinachohitajika kama sehemu ya mpango mzima wa ujenzi. Mojawapo ya majengo hayo ni nyumba za walimu, jengo la utawala kwa sababu lililopo halitoshelezi mahitaji, Maktaba ya kutosha kwa sababu iliyopo sasa haiwezi kuchukua wanafunzi wote kwa wakati mmoja na Zahanati kubwa ambayo itaweza kuisaidia mahitaji yote ya wanajumuiya ya Visiga na majirani kwa pamoja pia na nyumba za Mapadre na Masista.
ii. Ukarabati wa Majengo
Majengo yaliyopo mpaka sasa hapo Seminarini yanahitaji ukarabati mkubwa, Jimbo Kuu likishirikiana na uongozi wote wa Seminari lina mpango wa kukarabati majengo mbalimbali kama Madarasa, Maktaba, Nyumba za walimu, Mabweni, Nyumba za Mapadri na Masista, Bwalo la wanafunzi, Ukumbi wa Kanisa ili kuyaweka katika hali nzuri.
Utaratibu huu wa majengo unacheleweshwa na matatizo mbalimbali kama:
- Ujenzi usiokuwa wa kitaalam: Kabisa tangu mwanzo wa ujenzi wa seminari Jimbo limejikuta likihitaji fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo.
- Fedha: Kukosa fedha za kutosha kukarabati majengo hayo yote, kwani fedha zinazohitajika ni nyingi sana.
Haya ni matazamio ya Jimbo Kuu la Dar es salaam ambayo yalitolewa na Askofu wake Mkuu Polycarp Pengo tarehe 14 May 1997 Jimboni, katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu.
Uongozi chini ya Gombera wa saba Padre Eusebius Nzigilwa July 2003 - July 2008
Kwa mara ya pili, Padre Eusebius Nzigilwa anakuwa Gombera wa Seminari ya Visiga, akichukua nafasi ya Padre Mathias Mambo mara baada ya Mwenyezi Mungu kumuita kutoka katika makao haya ya dunia. Mpendwa Padre Mathias Mambo, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa kwa muda mrefu, alifariki dunia na kwenda kupumzika kwa amani kwa Bwana. Hivyo, Padre Eusebius Nzigilwa alichukua majukumu ya kuiongoza seminari kwa mara ya pili. Katika kipindi hiki, alihudumu kwa takribani miaka minne kabla ya kutumwa tena kwenda masomoni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako uteuzi wake wa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam ulimkuta mapema Januari 2010. Kwa miaka hiyo minne aliyoiongoza Seminari ya Visiga, mafanikio mbalimbali yalipatikana.
Uboreshwaji wa malezi kwa vijana katika Nyanja zote za kimalezi, kwa kipindi hiki ukomavu mkubwa kwa vijana katika maswala ya Kiroho, kiakili, kiutu na kinidhamu kwa ujumla wake vilishuhudiwa, aliyafanya na kuyaboresha haya kwa ushirikiano mkubwa na mapadre aliokuwa akifanya nao kazi; Padre Evarist Tarimo aliyekuwa makamu gombera na mlezi na mwangalizi wa nidhamu pamoja na Padre Desderius Rugemalira aliyekuwa baba wa kiroho wa seminari.
Aidha uongezwaji wa mifugo na uendelezwaji wa shamba la mahindi, pamoja na bustani za mbogamboga ulistawi zaidi katika kipindi hiki cha Uongozi.
Mafanikio makubwa ya kitaaluma katika kipindi hiki hayawezi kusahauliwa, kwani ni katika kipindi hiki ndipo seminari ya Visiga iliwahi kushika nafasi ya juu kabisa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa kushika nafasi ya pili kitaifa (Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2007)
Pia katika uongozi huu, palishuhudiwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa kikapu wenye hadhi na kupendeza, na pia ujenzi wa uwanja wa mpira wa mkono ( Volleyball pitch)
Aidha ni katika kipindi hiki walimu walijitosheleza kwa idadi kadiri ya mahitaji ya seminari, hii yote ilikuwa ni juhudi za wazi za Padre Eusebius Nzigilwa.
Uhusiano kati ya wawata na seminari ya visiga ulizidi kukomaa zaidi chini ya uongozi wa Padre Eusebius Nzigilwa.
Uongozi chini ya Gombera wa nane Padre Stephano Kaombe Aug 2008 - July 2013
Mara baada ya kutumwa masomoni kwa Padre Eusebius Nzigilwa, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alimtuma Padre Stephano Kaombe kuwa Gombera wa seminari ya Visiga. Kwa vipaji alivyojaliwa Padre Stephano Kaombe alifanya mambo mengi ya kukumbukwa katika seminari ya Visiga.
- Ukarabati wa kanisa la seminari na kulifanya kuwa lenye mvuto wa aina yake.
- Ujenzi wa Grotto la Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ikumbukwe msimamizi na mwombezi wa seminari ya Visiga ni Mama yetu Bikira Maria.
- Uchimbwaji wa bwawa la samaki na uanzishaji wa kufuga samaki katika bonde lililo katika eneo la seminari ulifanyika na matunda yake wana visiga wanayafaidi hadi hivi leo.
- Uwekwaji wa mfumo wa uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya jua, na hivyo kupunguza gharama za matumizi ya umeme uliotokana na Tanesco.
- Uanzishaji wa mfumo wa maji safi na salama kwa kuchimba maji ya ardhini ikiwa ni mradi mkubwa wa seminari kuwahi kufanyika katika kipindi chake. Mpaka sasa jumuiya ya seminari inatumia maji yake na kuacha matumizi ya maji toka Mamlaka ya usambazaji wa Maji (DAWASCO).
- Ukarabati wa madarasa kwa kuweka sakafu ya telezo.
- Ujenzi wa vyoo vya wanafunzi karibu na maabara.
Pia ni katika uongozi wa Padre Stefano Kaombe, seminari ilifanikiwa kupata gari nyingine kwa matumizi ya seminari; Land Cruiser hard top.
Katika uongozi huu hatuwezi kuwasahau Padre Dennis Ngumba aliyefanya kazi kama Makamu wa Gombera na pia alifanya kazi kama Padre mlezi na mwangalizi wa karibu wa miradi ya seminari, Padre Pesambili Masamba aliyefanya kazi kama Baba wa kiroho wa seminari.
Uongozi chini ya Gombera wa tisa Padre Dennis Ngumba
Hakika uongozi wa Padre Dennis Ngumba katika Seminari ya Visiga ulikuwa wa kipekee na wa kuigwa. Akiwa bado kijana mwenye maono mapana na moyo wa utumishi, alionyesha uzalendo wa kweli katika kuhakikisha maendeleo ya seminari yanaendelea licha ya changamoto mbalimbali zilizokuwepo. Padre Dennis, ambaye alikuwa msaidizi wa Gombera wakati wa uongozi wa Padre Stefano Kaombe, alipopewa jukumu la kuwa Gombera mkuu, alilikubali kwa unyenyekevu mkubwa na moyo wa kujitoa. Aliendeleza kwa moyo wa kujituma jitihada zote zilizokuwa zimeanzishwa na watangulizi wake, huku akiongeza msukumo mpya wa kiuongozi unaozingatia nidhamu, maendeleo ya miundombinu, na ustawi wa kijumla wa seminari kweny sekt ya elimu na kiroho.
Katika kipindi chake cha uongozi, Padre Dennis Ngumba alisimama imara kama kiongozi mwenye maono ya mbali, aliyetanguliza ustawi wa wasemnari kiroho , elimu na mazingira bora ya malezi ya kipadre. Mojawapo ya mafanikio yake makubwa ni ushirikiano mzuri aliokuwa nao na jumuiya nzima ya Seminari ya Visiga pamoja na alumni (waseminari wa zamani wa visiga) . Ushirikiano huu ulizaa matunda makubwa sana, hasa katika maboresho ya miundombinu ya seminari. Kwa mfano, alipambana kuhakikisha kuwa bwalo (Dining hall) ambalo lilikuwa katika hali mbaya sana linakarabatiwa na kurejeshwa katika hali nzuri inayofaa kwa matumizi ya kila siku ya chakula kwa waseminari. Kabla ya ukarabati huo, jengo hilo lilikuwa na mapungufu mengi kama paa kuvuja, sakafu iliyochakaa, na mazingira ya usafi yaliyohitaji maboresho ya haraka. Kwa msaada mkubwa kutoka kwa alumni wa Seminari ya Visiga pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya kanisa, aliweza kusimamia na kufanikisha ukarabati huo kwa mafanikio makubwa.
Zaidi ya hapo, Padre Dennis alielekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha uhifadhi bora wa chakula ndani ya seminari. Aliona umuhimu wa kuwa na vifaa imara vya kisasa vya kuhifadhi nafaka kama vile mahindi, mchele, maharage na vyakula vingine vya muda mrefu. Kwa kushirikiana na Visiga alumni , WAWATA pamoja na wafadhili waliokuwa na moyo wa kusaidia maendeleo ya seminari, aliweza kupata vifaa vya kuhifadhi nafaka ambavyo vilisaidia sana kupunguza upotevu wa chakula na kuhakikisha kuwa chakula kinatunzwa katika mazingira salama na ya kiafya. Hatua hii ilichangia sana kuboresha hali ya lishe kwa wanafunzi na pia kupunguza gharama za ununuzi wa mara kwa mara wa vyakula kutokana na upotevu wa awali.
Mafanikio haya ya uongozi wake yalikuwa ya wazi, na hata walimu pamoja na watumishi wengine wa seminari walithibitisha kuwa Padre Dennis alikuwa kiongozi aliyejitolea kwa dhati. Hakuwa tu gombera wa kiutawala, bali pia mlezi wa maisha ya kiroho, aliyesimama pamoja na mapadri wake akiwemo Padre Philip Tairo aliyekuwa Makamu wa Gombera, Padre Pascal Kamugisha aliyekuwa Baba wa Kiroho, na Padre Cletus Mzeru ambaye alisimamia miradi ya seminari kwa ukaribu. Hawa wote kwa pamoja walifanya kazi kwa mshikamano mkubwa na kuhakikisha kuwa ndoto ya maendeleo ya seminari inatimia chini ya usimamizi wa Padre Dennis.
Aidha, Padre Dennis hakujikita tu katika miundombinu bali pia alizingatia nidhamu ya kimasomo na kiroho ya waseminari. Alihimiza ibada za mara kwa mara, kujifunza kwa bidii, na malezi ya kipadre yenye msingi wa maadili mema. Alikuwa karibu sana na wanafunzi, akijenga uhusiano wa karibu wa mlezi na wanafunzi, hali iliyosaidia kuwawezesha waseminari kumweleza changamoto zao na kupata msaada wa kiroho na kimwili. Uongozi wake ulikuwa na falsafa ya kuwalea viongozi wa Kanisa la baadaye kwa moyo wa kujitolea, unyenyekevu, na maadili bora.
Katika mazingira ya changamoto kama ukosefu wa rasilimali za kutosha, Padre Dennis aliweza kutumia mbinu za ubunifu na ushawishi mzuri kushirikisha wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa maendeleo ya seminari hayaathiriki. Alitumia nguvu ya alumni kwa njia chanya, akiwahamasisha kushiriki katika kujenga seminari yao waliyoipenda na kuilea kwa miaka mingi. Ushirikiano huu uliibua ari mpya ya uzalendo miongoni mwa waseminari wa zamani ambao walijitokeza kwa moyo mmoja kusaidia katika miradi mbalimbali kama vile ukarabati wa bweni, uchangiaji wa vitabu vya kiada, na hata misaada ya kifedha kwa seminari.
Kwa ujumla, uongozi wa Gombera Padre Dennis Ngumba ulikuwa wa kipekee na wa aina yake, si tu kwa sababu ya jitihada na ufanisi wake mkubwa katika kusimamia Seminari ya Visiga, bali pia kutokana na ukweli kwamba yeye mwenyewe ni miongoni mwa alumni wa seminari hiyo. Hii ilimpa faida ya kipekee ya kuielewa vyema historia, mazingira, changamoto, na mahitaji halisi ya seminari hiyo, kwani aliwahi kulelewa na kusomea hapo. Kupitia uzoefu wake binafsi wa maisha ya seminari, Padre Dennis aliweza kuongoza kwa uelewa wa ndani, huruma, na moyo wa kujitolea uliotokana na mapenzi ya dhati kwa seminary aliyosoma.
Mwaka 2015, akiwa bado kwenye utume wake, aliteuliwa kuendelea na masomo ya juu ya kitaaluma, hali iliyosababisha kuhamishwa kwake rasmi kutoka nafasi hiyo. Hata hivyo, Ni wakati huo ndipo Padre Philipo Tairo, aliyekuwa Gombera Msaidizi aliteuliwa kuwa Gombera mkuu
Uongozi chini ya Gombera wa kumi Padre Philip Tairo
Baada ya uongozi wa Padre Dennis Ngumba, Baba Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo alimteua Padre Philip Tairo kuwa Gombera wa kumi wa seminari ya Visiga. Padre Tairo anaipokea seminari ya Visiga na kufanya baadhi ya miradi huku ikiwa katika maandalizi ya kufanya kumbukumbu ya Jubilee ya miaka ishirini na mitano (25). Hivyo kazi ilikuwa kubwa kwani sherehe iliambatana na uzinduzi mkubwa wa majengo mapya ya seminari na miundombinu yake.
Pia ni kipindi ambacho Baba Kardinali alizindua ujenzi wa majengo ya kidato cha tano na sita pia uzinduzi wa jengo jipya la Utawala .
Katika kipindi cha utumishi wa Pd. Philip Tairo kama Gombera wa seminari, mchango wake uliungwa mkono na Pd.Raymond Mbaula aliyekuwa Gombera Msaidizi, pamoja na Pd. Gasper Basilidi aliyekuwa baba wa kiroho wa waseminari. Wote hawa walifanya kazi kwa bidii na moyo wa kujitolea katika kulea na kuwasaidia vijana kuutambua na kuuendeleza wito wao. Hata hivyo, kwa sasa mapadre hao wote wamepangiwa utume katika maeneo mengine ndani ya Jimbo, na sasa uongozi wa Visiga Seminary unaendelea pamoja na Pd Manfred Semda (ACADEMIC DEAN) , Pd Paul Mamboleo (discipline master) na Pd Innocent Byemelwa (spiritual father) pamoja na watawa akiwemo Sister Edimondina ambaye amehudumu kwa muda mrefu sana seminarini kama mtawa na mwalimu bila kusahau watawa wengine ambao wamehudumu katika seminari kwa nyakati tofauti
Kwa vipaji alivyojaliwa Padre Philip Tairo anaendelea kufanya mambo mengi ya kukumbukwa katika seminari ya Visiga:
Ukarabati wa mabweni ya wanafunzi
Katika uongozi wa Gombera Padre Philipo Tairo, mojawapo ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni ukarabati wa mabweni ya wanafunzi, ambapo mabweni hayo yalifanyiwa marekebisho makubwa na kuwekewa madirisha mapya ya vioo. Kabla ya ukarabati huo, mabweni yalikuwa yamechakaa sana – madirisha mengi yalikuwa yamevunjika, sakafu zilikuwa zimeharibika, na mazingira kwa ujumla hayakuwa rafiki kwa malezi ya kitaasisi ya kipadre. Hali hiyo ilileta changamoto si tu kwa wanafunzi waliopo bali pia kwa taasisi katika suala la usajili wa wanafunzi wapya, kwani mazingira duni yalikuwa yanawakatisha tamaa baadhi ya wazazi na walezi waliotaka kuwapeleka watoto wao seminari.
Ukarabati huu uliokuja chini ya uongozi wa Padre Philipo Tairo uliibua sura mpya ya Seminari ya Visiga. Mabweni yaliyokuwa yamechakaa yamebadilika kuwa na mwonekano wa kisasa, safi, salama na rafiki kwa makuzi ya waseminari. Uwekaji wa madirisha ya vioo umeongeza mwanga wa asili, hewa safi, na hali ya utulivu kwa wanafunzi, hivyo kuboresha mazingira ya kusomea, kuishi, na kutafakari.
Moja ya matokeo makubwa ya ukarabati huu ni ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kila mwaka. Kwa kuwa miundombinu imeboreshwa, idadi ya waseminari wanaopokelewa imeongezeka kwa sababu sasa kuna nafasi ya kutosha ya kuwahifadhi kwa usalama na staha. Pia, wazazi na walezi wameanza kuwa na imani zaidi na taasisi kutokana na mazingira bora yanayochochea nidhamu na malezi ya kiroho.
Ujenzi wa jengo jipya la utawala
Moja ya matokeo makubwa ya ukarabati huu ni ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kila mwaka. Kwa kuwa miundombinu imeboreshwa, idadi ya waseminari wanaopokelewa imeongezeka kwa sababu sasa kuna nafasi ya kutosha ya kuwahifadhi kwa usalama na staha. Pia, wazazi na walezi wameanza kuwa na imani zaidi na taasisi kutokana na mazingira bora yanayochochea nidhamu na malezi ya kiroho.
Jengo hilo linajumuisha ofisi ya walimu wote wa seminari, ambapo kila mwalimu ana sehemu yake ya kufanyia kazi kwa utulivu na ufanisi. Vilevile, lina ofisi za mapadri wanaolea waseminari, academic dean, gombera, baba wa kiroho na wasaidizi wao, hivyo kuwezesha uratibu mzuri wa shughuli za malezi ya kiroho na kijumla kwa waseminari. Aidha, dining room ya walimu imejengwa katika jengo hilo, ikiwapa walimu sehemu maalum, safi na tulivu ya kupata chakula chao, jambo ambalo linaongeza heshima na kuonyesha kuthaminiwa kwao kama sehemu muhimu ya taasisi.
Mbali na hayo, jengo hilo lina nafasi kubwa inayoweza ku-accommodate walimu wengi, ikiwa ni pamoja na kumbi za mikutano na vyumba vya maandalizi ya masomo. Pia limewekewa vifaa bora vya kisasa kama vile kompyuta, printer, na vifaa vingine vya teknolojia ya habari na mawasiliano vinavyowawezesha walimu na mapadri kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. Katika jengo hilo pia ipo ofisi kubwa ya Rector (Gombera), yenye nafasi ya kutosha kwa mikutano, ushauri wa waseminari, pamoja na kushughulikia masuala ya kitaasisi kwa weledi na nidhamu kubwa.
Kwa ujumla, jengo hili la utawala limekuwa chachu kubwa ya maendeleo ya malezi bora ya waseminari. Kupitia jengo hili, walimu wamepata mazingira rafiki ya kufundishia, ambapo wanaweza kuandaa masomo yao kwa utulivu, kushirikiana kitaaluma, na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa ukaribu zaidi. Mazingira bora ya kazi huwapa walimu motisha na ari ya kujitolea, kwani wanahisi kuthaminiwa, kuheshimiwa, na kuwekewa miundombinu bora ya kutekeleza majukumu yao.
Pia, kwa kuwa malezi ya kipadre yanahitaji mshikamano wa walimu, mapadri na wanafunzi, jengo hili limekuwa kiungo kikuu cha kuimarisha ushirikiano huo. Kwa sasa, mawasiliano kati ya walimu na viongozi wa seminari yameimarika, utendaji wa shughuli za kila siku umeboreshwa, na wanafunzi wanapata huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Hakika, ujenzi wa jengo hili jipya la utawala ni alama ya uongozi makini wa Padre Philipo Tairo na uthibitisho wa jinsi gani miundombinu bora inaweza kuleta mabadiliko chanya katika mfumo mzima wa malezi ya kipadre. Ni urithi unaoendelea kuwanufaisha wengi na utaendelea kuwa msingi imara wa mafanikio ya Seminari ya Visiga kwa miaka mingi ijayo.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa madarasa na mabweni ya kidato cha tano na sita
Katika kipindi cha Gombera Padri Philip Tairo, alifanikiwa kuanzisha rasmi masomo ya kidato cha tano na sita katika Visiga Seminary. Hatua hii muhimu ilifikiwa baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa madarasa na mabweni ya kisasa yaliyokusudiwa kuwahudumia wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Masomo hayo yalizinduliwa rasmi na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo katika tukio la kipekee lililokwenda sambamba na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Visiga Seminary tangu kuanzishwa kwake.
Kuanzishwa kwa elimu ya juu ya sekondari (A-Level) katika seminari hii kumekuwa na mchango mkubwa katika kulea na kuimarisha miito ya kipadre miongoni mwa vijana waliopitia Visiga Seminary. Hali hii imepelekea ongezeko la mafrateri wanaoendelea na malezi ya kipadre katika majimbo mbalimbali hapa nchini. Mafanikio haya ni ishara ya matunda chanya ya uwekezaji wa kijumuiya katika elimu ya juu ya sekondari ndani ya mazingira ya seminari.
Aidha, hatua ya kuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita imeongeza ari kwa wanafunzi wanaotoka katika shule za sekondari za msingi (O-Level), kwani sasa wana nafasi ya kuendeleza masomo yao ndani ya mazingira yenye mwongozo wa kiroho, nidhamu ya hali ya juu, na malezi bora yanayoambatana na maadili ya Kikristo.
Mradi huu pia umeongeza hadhi ya Visiga Seminary kama taasisi ya malezi ya kitume na kielimu, na umefungua milango kwa vijana wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali za nchi kujiunga na safari ya kumfuata Kristo katika maisha ya kipadre.
Ujenzi wa miundombinu mipya seminari ya Visiga
Katika jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunza, kuishi na kutoa huduma, Seminari ya Visiga imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu mipya. Miradi hii ilijumuisha ujenzi wa majengo ya kisasa kwa ajili ya mradi wa mifugo wa seminari, ujenzi wa majengo ya Zahanati ya Visiga, na ukarabati wa maabara ya sayansi ili kuboresha elimu ya sayansi kwa wanafunzi.
Ujenzi wa majengo ya mradi wa mifugo ni sehemu ya mkakati wa seminari wa kujitegemea kiuchumi, ambapo wanafunzi pia hupata stadi za maisha zinazohusiana na ufugaji wa kisasa. Mradi huu husaidia katika uzalishaji wa maziwa, nyama na bidhaa nyingine za mifugo, ambazo hupunguza gharama za uendeshaji wa seminari na kuchangia lishe bora kwa wanafunzi.
Uboreshaji wa baadhi ya majengo ya Zahanati ya Visiga umeleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wanafunzi wa seminari, wafanyakazi na jamii inayowazunguka. Zahanati hii inaendelea kutoa huduma muhimu kama matibabu ya jumla, chanjo, huduma za afya ya uzazi na ushauri wa afya kwa walengwa mbalimbali. Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha afya ya wanafunzi na jamii inayowazunguka inalindwa na kuboreshwa.
Ukarabati wa maabara ya sayansi ni jitihada nyingine kubwa ambayo imeleta maboresho makubwa katika ufundishaji wa fizikia, kemia na baiolojia. Maabara sasa imewekewa vifaa vya kisasa vinavyowawezesha wanafunzi kufanya majaribio kwa ufanisi, hivyo kupata uelewa wa kina wa dhana mbalimbali za kisayansi. Hii husaidia kuboresha ufaulu na kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu bora katika nyanja za sayansi.
Kwa ujumla, maendeleo haya ya miundombinu yameboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Seminari ya Visiga na kuimarisha huduma za kijamii kwa wakazi wa maeneo ya jirani. Ni hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu na ustawi wa kielimu, kiafya na kiuchumi kwa seminari na jamii kwa ujumla.
Ujenzi na ukarabati wa kanisa la seminari ya Visiga
Ujenzi na ukarabati wa Kanisa katika Seminari ya Visiga ni hatua kubwa na ya msingi katika kukuza maisha ya kiroho ya waseminari na jamii yote ya seminari. Kanisa hili, ambalo sasa limekarabatiwa na kupanuliwa, limekuwa kituo cha sala, ibada, tafakari na mafundisho ya kiroho kwa vijana wanaojiandaa kwa upadre mtakatifu.
Uwepo wa kanisa zuri, lenye utulivu, uzuri wa kidini na miundo inayosaidia ibada, umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya waseminari wanaoandikishwa kila mwaka. Kanisa hili siyo tu mahali pa sala, bali ni shule ya kiroho ambapo waseminari hufundwa maadili ya Kikristo, nidhamu ya Kikatoliki na upendo kwa Mungu na jirani. Hii imeweka msingi imara wa malezi ya mapadre wema wa baadaye.
Msingi wa padri mzuri haujengwi tu juu ya maarifa ya kitaaluma, bali zaidi juu ya maisha ya sala, tafakari na ushiriki wa kila siku katika liturujia takatifu. Hivyo basi, kanisa hili limekuwa kituo cha malezi ya kiroho, mahali ambapo waseminari hujifunza maana ya toba, unyenyekevu, kujitoa na huduma ya kweli. Ni hapa wanapojifunza kusimama madhabahuni kwa heshima na ibada, wakiandaliwa kuwa wachungaji waaminifu wa watu wa Mungu.
Zaidi ya hayo, ukarabati wa kanisa umeongeza mwamko wa imani hata kwa waumini wanaoishi jirani na seminari, ambao hushiriki Misa na ibada mbalimbali pamoja na waseminari. Ushirikiano huu umeimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza utume wa Kanisa katika mazingira ya Visiga.
Kwa ujumla, kanisa hili ni msingi thabiti wa malezi ya kiroho kwa waseminari. Ni mahali ambapo mioyo ya vijana huundwa kuwa tayari kuitikia wito wa Mungu, kuishi kwa uaminifu katika upadre mtakatifu na kuwahudumia waamini kwa hekima, huruma na bidii.
Ujenzi wa nyumba ya kisasa ya mapadri
Ujenzi wa nyumba ya kisasa ya mapadri katika Visiga Seminary ni moja ya mafanikio makubwa yaliyolenga kuboresha makazi na mazingira ya huduma kwa mapadri wanaohudumu katika seminari hiyo. Nyumba hii ya kisasa imejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya kiroho, kijamii na kitaaluma ya mapadri, ikiwa na nafasi za kutosha, vifaa vya kisasa, na mazingira tulivu yanayowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Nyumba hii imejengwa kwa ubora wa hali ya juu, ikiwa na ofisi, vyumba vya kulala vya kutosha, jiko, sehemu ya mapumziko, na chumba maalum cha maombi au tafakari. Ujenzi huu umezingatia pia faragha na utulivu unaohitajika katika maisha ya kipadre, hivyo kuwawezesha mapadri kujitolea kikamilifu katika malezi ya waseminari, ushauri wa kiroho, na huduma nyingine za kichungaji.
Madhumuni ya ujenzi huu ni kuimarisha ustawi wa mapadri ili waweze kuwahudumia waseminari kwa moyo na hali bora zaidi. Kwa kuwa mapadri ni walezi wa kiroho wa waseminari, ni muhimu nao kuwa na makazi bora yanayochangia ustawi wao wa kimwili, kihisia, na kiroho. Nyumba hii imewapa nafasi ya kuishi kwa amani, kujiandaa kwa mafundisho, na kuwa karibu zaidi na Mungu katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, ujenzi wa nyumba hii unaonesha wazi kuthaminiwa kwa huduma ya mapadri na mchango wao mkubwa katika kulea viongozi wa Kanisa la kesho. Ni alama ya mshikamano wa kijumuiya na utambuzi wa kwamba mapadri pia wanahitaji mazingira bora ya kuishi ili kutekeleza kikamilifu wito wao wa kiutumishi.
Mafanikio
Mafanikio ya Visiga Seminary ni dhahiri na ya kujivunia, ambapo kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni, asilimia 99% ya wanafunzi wanaosoma katika seminari hiyo wamekuwa wakifaulu kwa kiwango cha juu katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne na kidato cha sita. Takwimu hii inaonesha ubora wa elimu inayotolewa, nidhamu ya wanafunzi, pamoja na juhudi kubwa za walimu na walezi wa kiroho katika kuhakikisha kuwa waseminari wanapata malezi bora kitaaluma na kiroho.
Changamoto
Changamoto kubwa inayojitokeza katika Visiga Seminary ni asilimia 30 tu ya waseminari wanaohitimu kidato cha sita wanaoendelea na masomo ya kilatini na falsafa kwa ajili ya safari ya upadri. Hii inaonesha kuwa, japokuwa idadi kubwa ya wanafunzi hufaulu vizuri kitaaluma, ni wachache wanaochukua hatua ya kuendeleza wito wao wa kipadre. Sababu mbalimbali zinaweza kuchangia hali hii, ikiwemo mabadiliko ya maamuzi ya mtu binafsi, mvuto wa fursa nyingine za kimaisha, au kukosa uhakika wa wito wa ndani.